SIKU YA TATU ZIARA YA MAKAMU WA RAIS MKOANI SONGWE

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Utawala Bora ni moja ya ahadi waliyoitoa kwa wananchi wakati wa kampeni.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Tunduma ikiwa ni siku ya nne ya ziara yake katika mkoa wa Songwe.

 “Lazima tunapofanya kazi zetu sheria zifuatwe, unapoacha kufuata sheria kwasababu ya Matakwa binafsi, kwasababu ya kunufaika wewe binafsi hili ni Tatizo hapa hapana utawala bora” 

Makamu wa Rais alisema Utawala bora usisukumwe tu upande wa Serikali unapaswa kupimwa kwenye ngazi zote mpaka za chini zikiwemo ngazi za Udiwani.

Makamu wa Rais amesisitiza kuwa Utawala bora ni pamoja na maendeleo ya Serikali yanapatikana.

Makamu wa Rais amesema Serikali itajenga pamoja na kuboresha vituo vya Afya 9 katika mkoa wa Songwe ambapo wilaya ya Momba kutakuwa na vituo vitatu.

Mapemaleo; Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amefungua kituo cha Afya cha Tunduma kilichofanyiwa maboresho na kugharimu zaidi ya shilingi milioni 500 naambacho kitahudumia wakazi zaidi ya elfu 80.

“Naomba sana Wananchi wa Tunduma pimeni Afya zenu, Serikali imetumia pesa nyingi kuweka mashine pale, kuweka mambo yote ambayo yanapaswa katika kutumika katika kupima afya, na naposema kupima afya simaanishi maradhi ya ukimwi peke yake lakini mashine zile zina pima mambo mengi”alisema Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais amesema upatikanaji wa Dawa ndani ya mkoa wa Songwe umekuwa kwa kiasi kikubwa.

Makamu wa Rais ameutaka Uongozi wa mkoa kuwasaidia kuwaendeleza vijana wajasiriamali ambao ni wabunifu na kuwasaidia kupata mikopo ya masharti nafuu.