Serikali yafuta vibali vya chuma chakavu vilivyokiuka sheria wadau waombe tena

Serikali imefuta vibali vyote vilivyokuwa vimetolewa kwa wafanyabiashara wa vyuma chakavu na biashara taka hatarishi kwa ujumla bila kufuata sheria na kuagiza mchakato wa utoaji vibali hivyo uanze upya ili kuhakikisha sheria ya mazingira inafuatwa.

Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene wakati wa Mkutano na wafanyabiashara wa vyuma chakavu uliofanyika leo Septemba 4, 2019 jijini Dar es Salaam.

Kutokana na hatua hiyo Mhe. Simbachawene amemugiza Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais kuunda haraka timu ya wataalamu kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa vibali vyote pamoja na vyuma chakavu vilivyokusanywa.

Alifafanua kuwa vibali vingine vimekuwa changamoto lukuki zikiwemo kutojulikana ukaguzi wake au kutumika kwa zaidi ya biashara moja jambo ambalo limekuwa likiikosesha mapato Serikali.

“Serikali hii ya wanyonge haina nia ya kumkomoa mtu katika hili la chuma chakavu tunawajali sana na ni biashara nzuri lakini ifikie kipindi tufuate utaratibu na kuwa na kibali maana tumebaini kuna dosari nyingi katika vibali vingi vilivyotolewa,” alisema.

Aidha kwa upande mwingine Mhe. Simbachawene alitangaza kuwa Serikali imerekebisha tozo ya vyuma chakavu ya sh. milioni 10 iliyokuwa inalalamikiwa na wafanyabiashara hao hasa wadogo na kufikia sh. milioni 5 hadi sh. laki 5.
Mhe. Simbachawene abainisha kuwa tozo hizo ni takwa la kisheria na haliwezi kujadiliwa au kubadilishwa hadi sheria ipelekwe Bungeni kujadili hivyo haitawezekana kuiondoa na kuwa Ofisi hiyo inaendelea kusimamia.