SERIKALI KUPAMBANA NA MIMEA VAMIZI NGORONGORO

Serikali imeazimia kurudisha ikolojia ya hifadhi ya Ngorongoro katika mazingira yake ya asili na kusisitiza kuwa shughuli zote za kuharibu na kuchafua  ikolojia hiyo vitadhibitiwa kwa nguvu na uwezo wote.

Akizungumza na Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba amesema kuwa lengo la ziara yake ni kufuatilia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa Mamlaka hiyo mwezi Machi 2017.

Katika ziara yake mapema mwaka jana pamoja na mambo mengine Waziri Makamba aliagiza Mamlaka hiyo kuchukua hatua za haraka na kuwaelekeza wamiliki wa hoteli na loji hususan zilizoko katika kingo za kreta katika bonde la Ngorongoro kutafuta vyanzo mbadala vya maji na kuondokana na kutegemea chanzo cha chemichemi za Lerai.

Aidha, Waziri Makamba aliagiza kuchukuliwa kwa hatua za haraka ili kudhibiti mimea inayohatarisha uoto wa asili katika Mamlaka ya Ngorongoro kwa kuunda jopo la wataalamu kutoka Tume ya Sayansi na Tecknolojia,  Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Hifadhi za Taifa za Tanzania, Wizara ya Kilimo na Mifugo na Mamlaka ya Ngorongoro ili kufanya utafiti wa kina na wakisayansi wa kubaini mbinu mpya ya kupambana na mimea hiyo vamizi inayotawala mimea inayotumiwa na wanyama kama malisho.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa maagizo hayo Kaimu Mhifadhi wa Ngorongoro Dkt. Maurus Msuha amesema kuwa Mamlaka ya Ngorongoro iliwaandikia barua wamiliki wote wa hoteli na loji  na kufanya tafiti kupitia kwa wataalamu elekezi wawili tofauti ambao kwa pamoja walishauri kuandaliwa kwa mkakati wa usimamizi na matumizi ya maji ndani ya Mamlaka ya Ngorongoro utakaokuwa suluhisho la matatizo la maji bila kuathiri mifumo ya ikolojia katika Hifadhi.

 

Aidha, katika kukabiliana na changamoto ya mimea vamizi ndani ya hifadhi, Bw. Msuha amesema kuwa Mamlaka imeanda ramani ya kuainisha aina, kiasi na maeneo ilipo mimea vamizi ndani ya hifadhi ili kuweza kuweka mikakati na mbinu sahihi za kukabiliana nayo ikiwa ni pamoja na kuendelea na kazi ya kutumia njia rafiki ya kimazingira ya kungo’a, kufyeka na kuchoma njia iliyoonyesha mafanikio makubwa hususan katika kudhibiti mmea tishio (Darura stramonium) ndani ya kreta na maeneo mengine.

 

Bw. Msuha amefafanua kuwa Ofisi yake inashirikiana na wataalamu wa Taasisi ya Sayansi na Teknoljia ya Nelson Mandela ya Mkoani Arusha na wameanziasha utafiti utakaodumu kwa kipindi cha miaka miwili, utafiti wa kuua magugu katika hifadhi kwa kutumia mifumo ya ki-biolojia. Matokeo ya awali yanaonyesha mafanikio kwa asilimia 70 katika kupambana na mimea vamizi.

 

Mara baada ya kupokea taarifa hiyo, Waziri Makamba amesema kuwa suala la mimea vamizi ni janga la kitaifa ambalo kwa sasa linawekewa mikakati ya kitaifa ili kuweza kukabiliana nalo. “Mimea hii vamizi imetapakaa maeneo mengi nchi hivyo jitihada za pamoja zinahitajika, Sisi Ofisi ya Makamu wa Rais tumeitisha Mkutano Mkubwa Arusha tarehe 04/09/2018 utaojumuisha wataalamu na wadau kutoka taasisi mbalimbali ili kwa pamoja tuzungumze chanzo cha tatizo hili, ukubwa wake, madhara na hatua za kuchukua” Makamba alisisitiza.

 

Pia, Waziri Makamba ametoa muda wa miezi mitatu kwa Mamlaka ya Ngorongoro kuanza kutekeleza kwa vitendo Mpango wa usimamizi na matumizi ya maji ndani ya Mamlaka na kutoa rai kwa wamiliki wa Hoteli na loji hususan zilizoko katika kingo za kreta katika bonde la Ngorongoro kuanza kuwekeza katika teknolojia ya kisasa ya kutibu maji taka ili yaweze kutumika tena na kuwataka kufahamu kwa matumizi ya maji kutoka ndani ya kreta hitimisho lake linakaribia.

 

Waziri Makamba yuko Mkoani Arusha kupitia utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa mwaka jana pamoja na kuzungumza na wadau waliowekeza katika hoteli na kambi za uwindaji.