Kiswahili | English
Site Keyword Search:
    
 
Total site visits: 3955093.MAKAMBA ATOA UFAFANUZI WA NYONGEZA YA MAMBO 11 YA MUUNGANO

Imebainika kuwa nyongeza ya mambo 11 ya Muungano yamefanyika kwa kufuata taratibu za kisheria na kwa mariadhano baina ya pande zote mbili za Muungano.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba wakati akijibu hoja za Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria hii leo mjini Dodoma.

Awali Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Saed Ahmed Kubenea akichangia taarifa ya iliyowasilishwa na Waziri Makamba juu ya Miradi inayotekelezwa Tanzania Zanzibar na ile ya Utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/18 na makadirio kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa fungu 26 na 31, alihoji namna mambo ya Muungano yameongezeka kutoka 11 hadi kufika 22.

Akijibu hoja hiyo Waziri Makamba alitumia fursa hiyo kufafanua kwa kina jinsi nyongeza ya mambo hayo ilivyofanyika kwa kusema jambo la 12 liliongezwa mara baada ya kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (East African Currency Body) mwaka 1964. Hivyo Serikali zote mbili zilikubaliana masuala hayo yashughulikiwe na Serikali ya Muungano.

Aidha, tarehe 11 Agosti 1967 yaliongezwa mambo ya Leseni za Viwanda na Takwimu (Jambo la 13) na Elimu ya Juu (Jambo la 14) kupitia Sheria ya mabadiliko ya Muda ya mwaka 1965. Hata hivyo tarehe 22 Julai 1968 “Rasilimali ya mafuta, petroli na gesi asilia” liliongezwa kwenye orodha ya Mambo ya Muungano na kuwa jambo la 15.

Waziri Makamba amesema kuwa, Jambo la 16 ambalo ni Baraza la Mitihani la Taifa liliongezwa tarehe 22 Novemba 1973, mara baada ya kuvunjika kwa Baraza la Mitihani la Afrika Mashariki mwaka 1971. Pia, Usafiri wa Anga, Utafiti, Utabiri wa hali ya hewa na Takwimu pia yaliongezwa kama mambo ya Muungano.

“Kwa mara ya kwanza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ilifanyiwa marekebisho mwaka 1979 ili kuanzisha Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara baada ya kuvunjika kwa Mahakama ya Rufani ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1978. Marekebisho haya yalisababisha orodha ya mambo ya Muungano kubadilika kwa kuongezeka suala la Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” Makamba alisisitiza.

 

Vilevile, mabadiliko ya nane ya Katiba yaliyofanyika mwaka 1992 yalifuta mfumo wa chama kimoja cha siasa na kurejesha mfumo wa vyama vingi vya siasa hali iliyosababisha kuongezeka kwa jambo jingine la Muungano ambalo ni “Uandikishaji wa Vyama vya Siasa”. 

Waziri Makamba amesema kuwa utaratibu uliotumika katika kuongeza idadi ya mambo ya Muungano ni kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ilivyoelekezwa katika Ibara ya 98(1) (b) ikisomwa pamoja na Orodha ya Pili kwenye Nyongeza ya Pili ya Katiba ambayo imeweka masharti kuwa Mswada wa Sheria kwa ajili ya kubadilisha orodha ya mambo ya Muungano lazima kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Zanzibar.

 

Kamati ya Katiba na Sheria imepitia na kukubali Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa fungu 26 na 31.

 


 

<< View list of News and Events.