NAIBU WAZIRI SIMA AZUNGUMZA NA WATAALAMU ELEKEZI WA MAZINGIRA

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mwl. Mussa Sima hii leo amekutana na Wataalamu elekezi wa masuala ya Mazingira Nchini na kuwataka kufanya kazi kwa mujibu wa Sheria, Taratibu na Kanuni  zilizopo ili kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya viwanda katika kusuma gurudumu la Maendeleo

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Millenium Towers Waziri Sima amelielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini kufanya mabadiliko ya Kanuni itakayo weka sharti la wataalamu wote elekezi kufanya kazi zao chini ya makampuni ya wataalamu elekezi wa mazingira “Firms of environmental experts” tofauti na sasa ambapo baadhi wamekuwa wakifanya kazi bila kuwa na makampuni.

Naibu Waziri Sima amesema kuwa ili kwenda sambamba na Sera ya Uchumi wa Viwanda nchini, Serikali ya awamu ya 5 imefanya mabadiliko ya Kanuni za Tathmini ya Athari kwa Mazingira na kuipa kipaumbele miradi ya viwanda na ile yenye manufaa kwa Taifa kama vile miradi ya umeme vijijini na kilimo. “Awali mchakato mzima ulikuwa unachukua siku 149 lakini kwasasa baada ya mabadiliko ya Kanuni za EIA  mchakato mzima unachukua siku 74 tu” Sima alisisitiza.

Aidha, Naibu Waziri Sima ameagiza kuhuishwa kwa kanzi data itakayosaidia kutangaza kazi zinazofanywa na wataalamu elekezi wa mazingira kwa kuzingatia ubora wake ili kusaidia wawekezaji. “Kazi zitangazwe na anzisheni vipindi vya kuelimisha umma vitavyozungumzia utaratibu wa Tathmini ya Athari ya Mazingira, Tusiishie tu kutoa vyeti, kikubwa zaidi ni NEMC kusimamia utaratibu, ili data base irahisishe ufuatiliaji wa miradi mbalimbali.” Sima alisisitiza.

Naibu Waziri Sima amewakumbusha wataalamu elekezi wa Mazingira “environmental experts” kuwa wazalendo kwenye maandiko ya miradi na kutotumiwa na watu wengine ili kukwamisha Miradi  muhimu na yenye maslahi mapana kwa Taifa kwa kuandika maandiko yenye kupotosha kwa nia ya  kukwamisha Miradi kwa maslahi ya watu wachache.

Mhe. Sima amesisitiza kuwa “Maandiko yenye kupotosha “misleading statements” ni kosa la kitaaluma “professional misconduct” kwa mujibu wa Kanuni namba 32 na 33 za Kanuni za Mazingira (Usajili wa Wataalamu wa Mazingira) Kanuni za Mwaka, 2005 G.N NO. 348 za mwaka 2005.”

Nae Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wataalamu Elekezi wa Mazingira (TEEA) Bw. Anael Macha amemshukuru Naibu Waziri Sima kwa kuwakutanisha na kuweka mikakati ya kufanya kazi kwa weledi zaidi na kuweka mkazo wa kutoa elimu kwa Umma juu ya  umuhimu wa kufanya Tathmini ya Athari kwa mazingira.

Jumla ya wataalamu  elekezi wa Mazingira 341 wamehudhuria kikao hicho  kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.