NAIBU WAZIRI SIMA AZITAKA NCHI ZILIZOENDELEA KUTIMIZA WAJIBU WAO

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Ramadhani Sima (Mb.) amehutubia Mkutano wa 24 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi unaendeleo  Nchini Poland.

Katika hotuba yake, Naibu Waziri ameeleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoathirika zaidi na athari za mabadiliko ya tabianchi duniani. Athari hizi ni pamoja na ukame, mafuriko na kuongezeka kwa ujazo wa bahari, jambo ambalo huathiri zaidi wakazi wa mwambao wa bahari pamoja na shughuli zao za kiuchumi ambazo ni msingi wa maisha yao. Athari hizi zimethibitishwa pia katika taarifa maalumu ya kisayansi iliyotolewa na Jopo la Kimataifa la Wataalamu wa Mabadiliko ya Tabianchi kuhusu athari zitakazojitokeza iwapo joto la dunia litaongezeka zaidi ya nyuzi joto 1.5 (1.50C). Kwa sasa joto la dunia limeongezeka kwa nyuzi joto 0.85 kulinganisha na kipindi kabla ya mapinduzi ya viwanda. Mhe. Sima ameitahadharisha jumuia ya kimataifa kuhusu athari za ongezeko hili na kuitaka kuchukua hatua za haraka na za makusudi kukabiliana na hali hii.

Katika otuba yake Naibu Waziri ameeleza juhudi za Tanzania katika kukabiliana na changamoto hizi ambazo zinaendana na mpango wa maendeleo wa Taifa. Juhudi hizi ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), Mfumo wa usafiri wa mwendo kasi katika jiji la Dar es Salaam, ujezi wa barabara za juu (flyovers and interchange) na ujenzi wa bwawa la umeme wa maji katika mto Rufiji (Stiglers Gorge) ambao unatarajiwa kuzalisha umeme kiasi cha MW 2,115. Nishati hii ya umeme ambayo ni safi kimazingira itasaidia katika ukuaji wa uchumi wa viwanda, undeshaji wa treni za umeme na kurahisisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa matumizi ya majumbani. Aidha amebainisha kuwa hizi ni hatua muhimu katika kusaidia kupunguza uzalishaji wa gesijoto zinazochangia ongezeko la joto duniani.

Mhe. Sima amezitaka nchi zilizoendelea zitimize wajibu wao kwa mujibu wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi pamoja na Makubaliano ya Paris kwa kutoa michango ya fedha na kuwezesha upatikanaji wa teknolojia za kisasa kwa nchi zinazoendelea kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya Tabianchi.

Mhe. Mussa Sima yuko nchini Poland akiongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano  ulioanza tangu tarehe 2 na utamalizika tarehe 14 Desemba, 2018.