MWONGOZO KWA WAKAGUZI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA MAKAMU WA RAIS

 

MWONGOZO KWA WAKAGUZI NA WATEKELEZAJI WA KATAZO LA MIFUKO YA PLASTIKI KWA HALMASHAURI ZOTE

  1. Ukaguzi utafanyika madukani, magengeni, masokoni, kwenye supermarkets, ghalani, mipakani, viwandani na kwenye maeneo mengine zinakouzwa bidhaa.
  2. Wakati wote wakaguzi wajitambulishe na kuonyesha vitambulisho vyao kwa wahusika kwenye maeneo wanayoyakagua.
  3. Hairuhusiwi kumsimamisha mtu na kumpekua au kupekua mizigo yake ili kutafuta mifuko ya plastiki.
  4. Hairuhusiwi kuingia kwenye makazi ya watu au kusimamisha magari au vyombo vingine vya usafiri ili kutafuta mifuko ya plastiki.
  5. Iwapo magari au vyombo vingine vya usafiri vitasimamishwa kwa sababu nyinginezo na kukutwa na shehena ya mifuko ya plastiki, adhabu stahiki itatolewa kwa mujibu wa Sheria na wahusika wataelekezwa mahala mahsusi kwa kupeleka shehena hiyo.
  6. Atakayekutwa na kosa la kuendelea kuuza, kuhifadhi au kutumia mifuko ya plastiki ataelekezwa pa kuipeleka mifuko hiyo, atapigwa faini inayostahiki kwa mujibu wa Sheria na atasainishwa fomu kukubali faini hiyo na atapewa muda wa kuilipa, kama Sheria inavyoelekeza. Atakapokataa kusaini au kushindwa kulipa katika muda aliopewa, ndipo atafunguliwa mashtaka.
  7. Watakaotozwa na kulipa faini, watapewa risiti za Serikali kwa malipo hayo.
  8. Busara itumike katika utekelezaji wa katazo hili na matumizi ya nguvu, ikiwemo kuwapiga au kuwabeba na kuwaweka ndani watu, hayaruhisiwi.
  9. Watakaokaidi au kutotoa ushirikiano katika ukaguzi au kuzuia au kuhujumu utekelezaji wa Sheria au kuendelea kufanya makosa baada ya kuelekezwa au kupewa adhabu, watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali zaidi kwa mujibu wa sheria nyingine za nchi.

IMETOLEWA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS

23 MEI 2019