Makamu wa Rais kushiriki Mkutano wa 12 wa Dharura wa Umoja wa Afrika nchini Niger

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan atashiriki Mkutano wa 12 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (12thExtraordinary Session of Assembly of the African Union)  utakaofanyika Niamey, Niger tarehe7 Julai, 2019, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mkutano huu wa 12 umeitishwa kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali kuhusu Eneo Huru la Biashara Afrika (African Continental Free Trade Area – AfCFTA). Mkutano huo ni matokeo ya maamuzi ya Mkutano wa 32 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika mwezi Februari, 2019 mjini Addis Ababa, Ethiopia.  Aidha, Mkutano huo utatanguliwa na Mkutano wa 35 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika ambao utafanyika tarehe 4-5 Julai, 2019.

Ujumbe wa Makamu wa Rais unajumuisha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.), Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Balozi Mohamed Ramia pamoja na viongozi wengine waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Makamu wa Rais na ujumbe wake wanatarajia kurejea nchini Julai 10, mwaka huu.