Makamu wa Rais atoa wito wa usimamizi wa misitu kuhakikisha upatikanaji wa maji

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema tusipotunza na kusimamia misitu yetu tutakuwa tunahatarisha upatikanaji wa maji kwa matumizi ya kijamii, kibiashara na kuimarisha mazingira.

Mhe. Samia amesema hayo Julai 31 wakati akifungua Jukwaa la Usimamizi Bora wa Misitu kwa Upatikanaji wa Rasilimali Maji Endelevu jijini Dodoma.

Makamu wa Rais alisema takwimu zinaonesha kuwa kiasi cha upotevu wa misitu kwa sasa ni kikubwa na pasipo na jitihada tunaweza kujikuta misitu hiyo haipo tena.

“Sote tunajua mradi wa uzalishaji wa umeme Rufiji utetegemea mtiririko endelevu wa maji ikiwemo mito na madakio ambayo yanaanzia kwenye misitu na maeneo mengine,” alisema Mhe. Samia.

Alisema kuwa rasilimali misitu na maji vinachangia sana kuboresha maisha ya wananchi na kumarisha mifumo na huduma za kiikolojia ikiwemo mabadilko ya tabianchi.

Aidha, Mhe. Samia alitaka mamlaka husika zichukue hatua husika pamoja na kuwepo kwa mahitaji kuongezeka huku akisema Jukwaa hilo litasaidia Serikali katika juhudi zake za kujenga uchumi endelevu kwa lengo la kuboresha maisha ya watu.

“Lengo kuu la Jukwaa la Maendeleo Endelevu ni kuhamasisha maedneleo jumuishi na endelevu yanayozingatia utunzaji mzuri wa mazinra na matumizi bora ya rasilimali,” alisema.