MAKAMU WA RAIS AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA OFISI YAKE IHUMWA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Ofisi ya Makamu wa Rais itakuwa ya mfano katika kutunza mazingira.

Makamu wa Rais ameyasema hayo leo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Makamu wa Rais Ihumwa, Dodoma.

“katika kupamba maofisi yetu kwa miti sisi ni watu wa mazingira  kwetu kuwe mfano wengine wakipita waseme kaangalieni ofisi ya Makamu wa Rais kulivyo kwa hiyo miti yetu tuitunze na bustani zimwagiliwe” alisema Makamu wa Rais.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba amesema ofisi yake imejitahidi kwa kadri ya uwezo wake kutekeleza maelekezo waliyopewa pamoja na kupanda miti katika eneo hilo.

Wakati huo huo Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Joseph Malongo alimueleza Makamu wa Rais kuwa Wizara zote zimepewa kiasi sawa cha pesa hivyo Makatibu wa Kuu walikaa na kukubaliana mchoro utakaotumika kama ofisi.

 Akitoa maelezo kwa Makamu wa Rais, Katibu Kamati ya Taifa ya Kuratibu Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma Bw. Meshach Bandawe alisema kuwa tangia uamuzi ulivyopitishwa na Serikali ujenzi ulianza mara moja kwa ofisi 21 pamoja na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na taasisi zingine na Ofisi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na eneo linalojengwa ofisi hizo limeshalipiwa fidia, na umeme umeshasambazwa, kwa sasa majengo yanayojengwa ofisi za chini lakini kila kiwanja kina eneo la kujenga ghorofa.