MAKAMU WA RAIS AHUTUBIA MKUTANO WA ‘AFRICA NOW SUMMIT 2019’

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema ili kuibadili Afrika Viongozi wake lazima wawekeze kwa Vijana na Watoto. Makamu wa Rais ameyasema hayo leo wakati akihutubia kwenye mkutano wa Africa Now Summit 2019 jijini Kampala nchini Uganda.

“Viongozi lazima wahakikishe wanawekeza kwenye lishe bora ya watoto wanaozaliwa na kuhakikisha mifumo yetu ya elimu inalenga katika kutoa elimu bora na zenye kukuza vipaji ili kwenda sawa na ulimwengu wa teknolojia.”alisema Makamu wa Rais.

 Aidha Makamu wa Rais amesisitiza Afrika lazima iwekeze kwenye mipango itakayoleta maendeleo endelevu kwa vizazi vijavyo na si mipango kwa ajili ya chaguzi zijazo. Mkutano huo uliofunguliwa na Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni unalengo la kuwakutanisha Viongozi wa Afrika kujadili masuala mbalimbali ya utengamano katika kuleta maendeleo endelevu barani Afrika.

 Rais Museveni amesema kwa kipindi kirefu Afrika haijabadilika ni wakati wa kuboresha elimu, kuboresha bidhaa zinazoingia sokoni, kupanua soko la kimataifa ambalo kwa sasa limeonekana finyu na kuimarisha miundombinu na kutambua umuhimu wa Sekta Binafsi katika kuleta mabadiliko endelevu ya kiuchumi.

 Viongozi wengine walioshiriki wakati wa ufunguzi ni Rais wa Somalia Mhe. Mohamed Abdullahi Mohamed, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Naibu Rais wa Kenya Mhe. William Ruto na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Misri Mhe. Amr Nassar.