Majaliwa ahadharisha kuna uwezekano wa kuvua mifuko ya plastiki 400 kuliko samaki

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuna uwezekano mkubwa wa kuvua mifuko 400 ya plastiki na samaki wawili ifikapo mwaka 2030 iwapo hatua za kuhifadhi mazingira hazitachukuliwa.

Mhe. Majaliwa ametoa tahadhari hiyo Juni 28, 2019 wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge jijini Dodoma.

Alisema Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) inaonesha kufikia mwaka huo dunia itakuwa na mifuko mingi ya plastiki kwenye maji kuliko samaki na viumbe wengine.

Alisema Tanzania inajivunia uwepo wa rasilimali nyingi za asili zikiwemo wanyama na milima ambazo ni chachu ya uchumi wetu lakini zinaweza kutoweka kama hatutachukua hatua za kuzilinda.

Waziri Mkuu alibainisha kuwa Taarifa ya tatu ya hali ya mazingira ya mwaka 2018 inaonesha hali ya mazingira nchini si ya kuridhisha.

“Shughuli za kibinadamu zikiwemo ufyekaji misitu umekuwa wa ovyo kilimo kisicho endelevu na utupaji taka ovyo zikiwemo za plastiki vinatishia kuangamiza mazingira ya nchi,” alisisitiza.