KIKAO CHA WADAU KUHUSU FURSA YA UWEKEZAJI KATIKA UZALISHAJI WA MIFUKO MBADALA

MAELEZO YA AWALI YA NAIBU KATIBU MKUU, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, BALOZI JOSEPH E. SOKOINE KWENYE KIKAO CHA WADAU KUHUSU FURSA YA UWEKEZAJI KATIKA UZALISHAJI WA MIFUKO MBADALA, UKUMBI WA JULIUS NYERERE INTERNATIONAL CONVENTION CENTRE (JNICC), DAR ES SALAAM, TAREHE 06 NOVEMBA, 2018

Napenda kuchukua fursa hii muhimu kuwashukuru wote  kwa kuitikia wito na kufika kwenu katika kikao hiki muhimu licha ya majukumu mengine mliyonayo. Wingi wenu unanipa faraja na matumaini makubwa kuwa malengo ya kuitisha kikao hiki yatafanikiwa pasipo shaka. Mashauriano na ushirikiano ni moja ya nyenzo muhimu katika kufanikisha suala lolote lenye maslahi kwa taifa na manufaa kwa kizazi cha sasa na vijavyo.

Ndugu Washiriki,

Naomba nianze kwa kutoa maelezo machache ya utangulizi na hatimaye nigusie madhumuni  ya kikao hiki. Bidhaa za plastiki zilianza kutumika kwa wingi duniani kote katika miaka ya 1950. Bidhaa hizi zina matumizi mengi ikiwemo vifungashio vya vyakula, madawa na mbolea; samani za majumbani kama viti na meza; vifaa vya ujenzi kama vile mabomba ya maji na hata mavazi. Hata hivyo, zaidi ya nusu ya bidhaa hizi hutumika kama vifungashio au mifuko ya kubebea bidhaa, ambapo sehemu kubwa huishia baharini. Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira, zaidi ya asilimia 80 ya takataka zilizopo baharini hutokea nchi kavu. Inakadiriwa kuwa, kila maili moja ya mraba ya bahari ina vipande vya takataka za plastiki vinavyoelea takribani 46,000. Kila mmoja wetu hapa anahusika katika uchafuzi huu mkubwa wa bahari kwa namna moja au nyingine. Hali hii inachangia vifo vingi vya viumbe wa baharini.

Ndugu Washiriki,

Takwimu zinaonesha kuwa takriban nusu ya taka za plastiki zinazozalishwa zinajumuisha vifungashio na mifuko ya plastiki. Uwezo wetu wa usimamizi na udhibiti wa taka za plastiki ni hafifu. Hivyo, sehemu kubwa ya taka hizi huishia kwenye madampo na kuzagaa kwenye mazingira. Iwapo hali hii ya matumizi ya mifuko na vifungashio vya plastiki na usimamizi hafifu wa taka itaachwa iendelee tunakaribisha janga la mazingira katika miaka ijayo. Kwanini tunasema hivyo?

Vifungashio vya plastiki huchukua muda mrefu kuoza katika mazingira takriban miaka 500 hadi 1,000, kwa maneno mengine huchukua karne kadhaa kuoza katika mazingira. Hii inamaanisha kuwa vifungashio vyote vya plastiki vilivyozalishwa tangu miaka ya 1950 hadi leo bado viko katika mazingira kwa namna moja au nyingine na katika sehemu moja au nyingine. Je, tuache hali hii iendelee?. Tutafakari hali itakavyokuwa miaka 500 au zaidi ijayo. Tutarajie nini kuhusu rutuba ya ardhi (kilimo), uvuvi, utalii na mandhari ya mazingira yetu kwa ujumla? Ni dhahiri kwamba iko haja ya kuchukua hatua mahsusi kulingana na hali hii.

Ndugu Washiriki,

Isitoshe, vifungashio na mifuko ya plastiki ina changamoto nyinginezo ikiwemo kuzagaa ovyo katika mazingira; vifo vya mifugo wanapokula na kumeza mifuko hii; kuziba mitaro ya maji ya mvua, miundo mbinu ya maji na majitaka na kusababisha mafuriko na kuenea kwa magonjwa ikiwemo malaria na kipindupindu. Aidha, kwa kuwa mifuko hii huelea katika maji kwa muda mrefu huchangia katika kusafirisha vimelea vya magonjwa kutoka eneo moja hadi jingine. Hali kadhalika, imezoeleka kwa mama ntilie wanapopika hufunika vyakula kwa kutumia mifuko ya plastiki ambayo huhatarisha afya ya mlaji kutokana na uwezekano wa baadhi ya viambata vya sumu kufyonzwa kutoka kwenye mifuko kwenda kwenye chakula hasa katika hali ya joto. Naamini wote tunakubaliana kuwa afya ni uhai, hivyo tunapaswa kuchukua hatua kulinda afya ya jamii kwa manufaa yetu na ya taifa kwa ujumla.

Ndugu Washiriki,

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira linakadiria kuwa hali ya sasa ya uzalishaji na matumizi ya mifuko na vifungashio vya plastiki ikiendelea, ifikapo mwaka 2050 takataka za plastiki zitakuwa nyingi kuliko samaki baharini. Hii kwa upande mmoja inadhihirisha kuwa changamoto ya taka za plastiki si suala la afya ya jamii na hifadhi ya mazingira tu bali linagusa uchumi na mustakabali wetu wa maisha yetu ya sasa na ya vizazi vijavyo.

Changamoto ya udhibiti wa vifungashio na mifuko ya plastiki ya kubebea bidhaa ni suala la dunia nzima. Kwa kutambua hili, Kikao cha Pili cha Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mazingira wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (Second Session of the United Nations Environment Assembly of the United Nations Environment Programme) uliofanyika Nairobi, Kenya mwaka 2016, kupitia Azimio Na. UNEA 2/11, uliazimia kuwa uchafuzi wa taka za plastiki baharini ni changamoto ya Dunia inayohitaji hatua za haraka. Hivyo, ni muhimu kama Taifa tukashirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuchukua hatua madhubuti ili kuinusuru Dunia dhidi ya janga hili.

Ndugu Washiriki,

Baada ya maelezo hayo ya utangulizi, naamini taswira na madhumuni ya kikao cha leo imeeleweka. Kikao hiki kinalenga kupata mwelekeo wa kuchukua hatua muafaka ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaochangiwa na mifuko ya plastiki. Moja ya hatua hizo ni kuhamasisha uzalishaji na matumizi ya mifuko mbadala iliyo rafiki kwa mazingira ikiwemo ya karatasi, vitambaa vya nguo na hata vikapu vya asili. Hivyo, madhumuni ya kikao hiki ni kuwatambua wadau muhimu katika azma yetu ya kuleta mabadiliko yenye manufaa kwa afya ya jamii, hifadhi ya mazingira na uchumi kwa ujumla. Aidha, lengo muhimu zaidi la kikao hiki ni kujenga mazingira wezeshi kwa wadau kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa mifuko mbadala ili kurahisisha hatua za kudhibiti taka za plastiki hasa zile zitokanazo na mifuko ya plastiki.

Ndugu Washiriki,

Sote tunafahamu kwamba matumizi ya mifuko ya plastiki yameongezeka hasa kutokana na mifuko hii kutolewa bure kwenye maduka, masoko, migahawa na maeneo mbalimbali.  Aidha, kutokana na baadhi ya nchi jirani kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki na kuruhusu uzalishaji kwa ajili ya soko la nje ya nchi, pamekuwepo na wimbi kubwa la uingizaji wa mifuko ya plastiki hapa nchini ikiwemo kupitia njia zisizo rasmi.

Kama tunavyofahamu Serikali kwa muda sasa imekuwa ikifanyia kazi suala la kuzuia uzalishaji na matumizi ya mifuko ya plastiki ya kubebea bidhaa nchini. Dhamira hiyo bado ipo na inafanyiwa kazi na niseme kuwa kikao hiki ni moja ya hatua za kimkakati katika kufikia azma hiyo.

Ndugu Washiriki,

Kwa muktadha huu, uwekezaji katika mifuko mbadala ni fursa maridhawa kutokana na uwepo wa teknolojia zenye gharama nafuu na rahisi kwa mazingira yetu ya kiuchumi na kijamii. Hii ni fursa kwa wajasiriamali, vikundi vidogo vidogo na hata makampuni. Aidha, ni fursa kwa kila mmoja wetu maana mifuko mbadala iko mingi kuanzia mifuko ya karatasi, nguo, ukili na mingineyo. Hivyo, tunapaswa tuchangamke, kila mmoja kwa nafasi yake. Tumejumuika hapa ili kwa pamoja tujadili na kupeana hamasa ambayo ni muhimu ili kutoa motisha kwa wadau wote katika ngazi mbalimbali kuwekeza katika uzalishaji wa mifuko mbadala na hatimaye kuchangia katika utunzaji wa mazingira, kuboresha kipato binafsi na pato la taifa kwa ujumla. Fursa hii iko wazi kwa kila mmoja kwa nafasi yake, tusisite kwa vyovyote vile kwani pale penye dukuduku tunapaswa kuzungumza na kuweka mikakati ya pamoja. Aidha, nitoe angalizo kuwa ni muhimu bei ya mifuko mbadala ikawa nafuu na kwa kiwango ambacho wananchi wengi wanamudu.

Ndugu Washiriki,

Kama mlivyosikia kwenye utambulisho, kikao kinajumuisha wamiliki wa viwanda vinavyozalisha bidhaa za karatasi, wawakilishi wa sekta binafsi, waandishi wa habari na baadhi ya Wizara na Taasisi za Serikali.  Ninawaomba mjadala wetu tuuendeshe kwa uwazi na weledi ili uwe wenye tija na mafanikio kwetu sote.

“Mifuko Mbadala kwa Ustawi wa Afya, Mazingira na Uchumi Wetu” ndiyo kauli mbiu inayopaswa kutuongoza katika mjadala na mazungumzo yetu.

Baada ya kusema hayo, napenda sasa nitamke kuwa nimefungua rasmi kikao hiki. Mifuko Mbadala kwa Ustawi wa Afya, Mazingira na Uchumi Wetu!