HOTUBA YA WARSHA YA UDHIBITI NA USIMAMIZI WA KEMIKALI

HOTUBA YA MKURUGENZI – IDARA YA MAZINGIRA, Bi. ESTHER MAKWAIA, OFISI YA MAKAMU WA RAIS KATIKA WARSHA YA UDHIBITI WA KEMIKALI NA KEMIKALI TAKA KWA WADAU WA SEKTA YA MAFUTA NA GESI NCHINI YALIYOFANYIKA TAREHE 16-17 AGOSTI 2018 KWENYE UKUMBI WA BOT, DAR ES SALAAM

 Mheshimiwa Mkemia Mkuu wa Serikali,

Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Kemikali – Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali

Wawezeshaji na washiriki wa warsha,

Wawakilishi wa vyombo vya habari,

Mabibi na Mabwana.

Ninayofuraha kubwa kujumuika nanyi katika ufunguzi wa warsha ya udhibiti wa kemikali na kemikali taka kwa taasisi zinazohusika na udhibiti wa kemikali katika sekta ya mafuta na gesi, ilikulinda afya za wananchi na kuzuia uchafuzi wa mazingira.

Uamuzi wa kuwaita unatokana na kutambua umuhimu wa sekta hii nchini na ikizingatiwa kwamba sekta hii inatumia kemikali nyingi, na kuzalisha kemikali taka ambazo zinaweza kuleta madhara kwa afya na mazingira zisipodhibitiwa.

Warsha hii inafanyika ili kwenda sambamba na jitihada za Mh. Rais Dkt.  John Pombe Joseph Magufuli yakujenga uchumi wa kati na maendeleo ya viwanda.

Nichukue fursa hii, kwa niaba ya Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kuwashukuru sana Shirika la Umoja wa kimataifa la Mazingira Duniani  kwa kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania katika kufikia lengo la udhibiti wa kemikali na kemikali taka. Tunatarajia kuwa, Shirika la Umoja wa Kimataifa la Mazingira Duniani (UNEP) na umoja wa Mataifa kwa ujumla wataendelea kuwa nasi bega kwa bega tukiendelea na juhudi za kwenda nchi ya uchumi wa kati wa viwanda tunayoikusudia.

Ushirikiano wanaoonyeshwa ni udhihitisho tosha katika kujenga nchi yenye viwanda kama inavyoanishwa katika mkakati wa maendeleo wa 2025.

Ndugu Washiriki,

Matuimizi yake mikali huchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia dunia na ni vigumu kuyaepuka.

Kemikali hutumika kwenye maeneo mbalimbali katika maisha ya mwanadamu ikiwemo uzalishaji wa chakula, nguo, majisafi na salama, viwandani, mashuleni, mahospitalini, migodini, majumbani, n.k. Hata hivyo, wakati mwingine matumizi ya kemikali yanaweza kuleta madhara kwa afya na mazingira kama matumizi hayo hayatadhibitiwa. Wahusika wote hutakiwa kujua namna sahihi ya kutumia kemikali na kushughulikia kemikali –taka zinazozalishwa. Matitizo mbalimbali hutokana na sababu kadhaa zikiwemo uelewa mdogo wa sheria za nchi na ufinyu wa rasimali watu, hivyo kuchangia matumizi  yake kutumikali isivyo sahihi, na udhibiti hafifu wa kemikali taka. Udhibiti wa kemikali na kemikali taka ni muhimu katika kila sekta inayotumia kemikali ikiwemo sekta ya mafuta na gesi ambayo inakuwa kwa kasi nchini.

Ndugu Washiriki,

Kemikali zinazotumika katika sekta ya mafuta na gesi ikijumuisha shughuli zote za uingizaji, usafirishaji, usambazaji, utumiaji, uchimbaji, na utengenezaji wa mazao ya mafuta na gesi kama vile vilainshi, hutumika katika hatua mbalimbali kama vile usafirishaji, kuzuia kuziba kwa miamba, kuzuia kutu, kupunguza uoto wa wadudu n.k.

Kama ilivyo kwenye maeneo mengine, baadhi ya kemikali zinafahamika kuwa na madhara kwa afya na mazingira.  Kemikali kadhaa zinazotumika katika maeneo ya uchimbaji wa mafuta na gesi huweza kusababisha madhara kwa samaki na viumbe vingine vya majini, na kwenye mazingira.  Madhara pia huweza kutokea kwa afya za wafanyakazi kama wasipotumia vifaa kinga wakati wa utumiaji wa kemikali.  Endapo hatua stahiki hazitachukuliwa kuhakikisha matumizi salama ya kemikali na kemikali-taka madhara ya kemikali hizi yanaweza kuongezeka hasa katika kipindi hiki cha ukuaji wa sekta ya mafuta na gesi.

Ndugu Washiriki,

Kwa kutambua haki ya kikatiba ya kila mtanzania na azimio la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu ya kuhakikishiwa mazingira bora ya kuishi kwa afya na familia yake, Serikali imechukuwa hatua mbalimbali kudhubiti athari zinazoweza kutokea kutokana  na matumizi yasiyo salama ya kemikali na udhitibiti wa kemikali – taka. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuanzisha Sera ya mazingira, Sera ya Afya na Sera ya Kilimo, Sera ya mafuta na gesi. Kutunga sheria mbalimbali ikiwemo za udhibiti wa mazingira na udhibiti wa kemikali.

Lengo kuu la Sera, Sheria na Miongozo iliyoanzishwa ni kuhakikisha kuna kuwa na mfumo bora unaohakikisha shughuli hizi zinafanyika kwa usalama kwa afya na mazingira. Hatua hizi za serikali, zinaenda sambamba na mikataba na makubaliano ya kimataifa kama vile Mkataba wa Stockholm unaozungumzia udhibiti wa kemikali zinazodumu kwenye mazingira kwa muda mrefu na hivyo kuleta madhara kwa afya na mazingira.

Mkataba wa Minamata unahusu udhibiti wa Zebaki; Mkataba wa Rotterdam unahusu utaratibu wa biashara ya kimatifa ya kemikali na viuatilifu hatarishi na Mkataba wa Basel unaohusu udhibiti wa usafirishaji na utupati wa Taka za Sumu kati ya nchi na nchi.  Warsha hii ni mwendelezo wa jitihada za Serikali za kutimiza wajibu wake wa kulinda afya na mazingira ya wananchi, wakati shughuli za sekta ya gesi na mafuta zinaendelea.

Ndugu Washiriki

Serikali inatambua umuhimu wa sekta ya mafuta na gesi katika kufikia lengo la serikali la kujenga maisha bora kwa kila mtanzania, warsha hii inawaleta pamoja wawakilishi wa vyombo vya serikali vinavyohusika katika sekta ya mafuta na gesi, ili kuwapo na uelewa zaidi katika suala la udhibiti wa kemikali zinazotumika kwenye sekta hii.

Natarajia ifikapo kesho mtakuwa na ufahamu zaidi wa eneo hili.  Hivyo mtatoa mchango kufuatana na utaalamu na uzoefu wenu katika kuboresha mfumo wa udhibiti wa kemikali na kemikali – taka kwenye sekta ya mafuta na gesi nchini.  Serikali iko tayari kufanya kazi nanyi kwa karibu kuhakikisha kuwa sekta ya mafuta na gesi inakuwa kwa kasi bila kuathiri afya na mazingira ya wananchi.

Natarajia pia kuwa, warsha hii itawezesha ushirikiano wa karibu zaidi kati yenu, ili kutuhakikishia utekelezaji wa sheria mbalimbali mnazozisimamia.

Kwa maneno haya machache ya ufunguzi wa warsha, napenda kuwashukuru waandaaji wa warsha hii kwa kazi nzuri waliyofanya. Napenda sasa kutamka rasmi kuwa warsha hii amefunguliwa Rasmi.

 

Asanteni kwa kunisikiliza.