BWAWA LA URUGHU KUTANGAZWA KAMA ENEO LINDWA -MAKAMBA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba ameendelea na ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Iramba kwa kutembelea bwawa la Urughu na kuwataka wakazi wa eneo hilo kusimamia rasilimali hiyo kwa mustakabali wa maisha yao ili kuendeleza fursa zilizopo ikiwa ni pamoja na masuala ya uvuvi na kilimo.

Mhe. Makamba amesema ili bwawa hilo liweze kutangazwa kama eneo lindwa ki-mazingira ni lazima wananchi wawe na utashi, utayari na uwezo wa kutunza bwawa hilo kwa kufuata masharti yatakayotolewa katika tangazo la Serikali ikiwa ni miongoni mwa maeneo 77 yaliyopendekezwa kuhifadhiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira.

Waziri Makamba amesema uhifadhi wa bwawa hilo utaendana na makatazo kwa baadhi ya shughuli za kibinadamu ili kulinusuru ikiwa ni pamoja na kuzuia shughuli za uvuvi na kilimo kisicho endelevu katika Vyanzo vya maji. Aidha, Waziri Makamba ameutaka Uongozi wa Wilaya ya Singida kupitisha azimio lao la kuhifadhi bwawa la Urughu na Msitu wa Ushora katika Baraza la Madiwani.

Waziri Makamba ameahidi bila kuchelewa kutangazwa Bwawa la Urughu kuwa eneo nyeti kimazingira na kusaidia kuondoa kadhia ya kujaa kwa mchanga katika bwawa hilo. “Ili sisi tuendelee na mchakato huo tuleteeni sifa za maeneo husika kama vile, milima, mabwawa na mashamba yenye umuhimu mkubwa na historia inayojenga hoja ya umuhimu wa ulinzi katika eneo hilo, pia lipatikane azimio la Baraza la Madiwani kuwa ni eneo nyeti na kuwasilisha ombi ili Waziri aweze kuchukua nafasi yake kisheria” Makamba alibainisha.

Pia, Mhe. Makamba ametembelea Ziwa Kitangiri lililopo katika Kijiji cha Doromoni, Kata ya Tulya, Tarafa ya Kisiriri na kufanya mkutano wa hadhara na wakazi wa eneo hilo ambao wamepaza sauti juu ya changamoto inayowakabili ya kuhifadhi ziwa Kitangiri.

Diwani wa Kata ya Tulya Bw. Wilfred Kizanga amebainisha kuwa ziwa hilo linapakana na Wilaya za Meatu, Igunga na Kishapu ambazo amezituhumu kufanya shughuli zisizo endelevu katika ziwa hilo na kusabisha kina cha maji kupungua na kuendeleza uvuvi haramu. “Sisi wana – Doromoni kwa upande wetu tunahifadhi hili ziwa, tatizo ni wenzetu wa Wilaya tunazopakana nazo, shughuli zao za kibinadamu si endelevu” alifafanua Mhe. Diwani.

Akijumuisha ziara yake katika Wilaya ya Iramba Mhe. Makamba ameagiza Uongozi wa Wilaya kuuanda Kamati za Mazingira na kuahidi kutoa mafunzo kwa kamati zitakazoundwa ili kurahisisha shughuli za uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira wilayani hapo “Natarajia hadi mwezi Desemba kamati ziwe zimeundwa katika ngazi zote na ziwe mfano, Waziri Makamba alisisitiza”

Katika hatua nyingine Waziri Makamba ameahidi kutafuta mradi kwa ajili ya kuhifadhi Ziwa Kitangiri na kidakio cha maji ili kurejesha ziwa hilo katika hali yake ya awali. Mradi huo pia utasaidia kutoa mbadala wa shughuli zisizo endelevu pembezoni mwa ziwa na vyanzo vya maji vinavyopeleka maji katika ziwa hilo ili kurahisisha mchakato wa hifadhi ya ikolojia ya Mto Kitangiri.