AZISHENI KAMATI ZA MAZINGIRA – MAKAMBA

Jamii imetakiwa kufahamu kuwa Kamati za Mazingira katika ngazi zote zipo kwa mujibu wa Sheria, Sheria ya Mazingira kifungu Na. 38 (1-2) na Kamati hizo zina wajibu wa kusimamia mazingira kikamilifu yanayohusu maeneo yao.

Akizungumza na Watendaji wa Mkoa wa Tabora katika hafla ya kuzindua Kamati ya Usimamizi wa mazingira Mkoani hapo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba ameahidi kujenga uwezo kwa watendaji hao kwa kuwapatia mafunzo.

Aidha, Waziri Makamba amesisitiza unaziswaji kwa Kamati za Mazingira katika ngazi za vitongoji, vijiji na kata nchi nzima na kuahidi kutuma wataalamu kutoa mafunzo kwa kamati hizo ili ziweze kujua majumu yao ipasavyo na kusema kuwa shughuli za hifadhi za mazingira hazitafanikiwa kama Kamati za mazingira hazitatimiza majukumu yake katika ngazi hizo.

Waziri Makamba amesema kuwa dunia tunayoishi sasa tumeiazima kwa kizazi kinachokuja hivyo hatuna budi kuitunza. “Ukiazima kitu kwa mtu yeyote huna budi kukitunza na kukulinda ila kukirudisha kwa mwenyewe kikiwa katika hali nzuri.” Makamba alibainisha.

Katika wakati mwingine Waziri Makamba ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Tabora kuteua ama kuajiri Maafisa wa mazingira wa kutosha ili kusimamia kikamilifu uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira, pamoja na kuandaa mpango tekelezi wa mazingira katika ngazi ya Mkoa.

Kuhusu usimamizi wa taka, Waziri Makamba ametoa wito kwa uongozi wa Mkoa wa Tabora na Halmashauri zote kuwa na takwimu sahihi ya kiwango cha taka kinachozalishwa kwa siku ili taka hizo ziweze kutumia katika uzalishaji wa nishati. “Naagiza kila Halmashauri kufahamu kiwango cha uzalishaji wa taka, hii itasaidia kuja na miradi ya kuzalisha nishati mbadala pale fursa zitakapopatikana.” Makamba alisisitiza.

Katika hatua nyingine Waziri Makamba amesisitiza matumizi ya nishati mmbada kwa taasisi za Serikalini ili kupunguza kiwango cha ukataji wa miti na matumizi ya mkaa, pia amewataka wadau na wakulima wa tumbaku kubuni namna bora ya kuchoma tumbaku ili iweze kupata soko zaidi duniani. “Sote tunafahamu kuwa miti ni gharama, haiwezekani mkulima kuteketeza kiasi cha miti yenye thamani ya Shilingi laki mbili kuzalisha tumbaku ya elfu themanini, hii haikubaliki ni lazima tubadilishe uchomaji wake”. Waziri Makamba amebainisha.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri amemueleza Waziri Makamba jinsi Mkoa wake unavyotekeleza kikamilifu kampeni ya upandaji miti kwa kuwa na kauli mbiu ya ‘Tabora ya Kijani’ na  amemshukuru Waziri Makamba kwa kufanya ziara katika Mkoa wake na kuahidi kutekeleza agizo la kuteua maafisa wenye sifa ya kuwa wakaguzi wa Mazingira.

Waziri Makamba amehitimisha ziara yake Mkoani Tabora kwa kutembelea Bwawa la Igombe na Kazima ili kuona utashi na utayari wa wananchi katika kuhifadhi maeneo hayo kabla ya kutangazwa katika gazeti la Serikali kama eneo lindwa. Akiwa Kijijini Igambilo Mheshimiwa Makamba ameahidi kutoa mifuko 100 ya Saruji kuchangia ujenzi wa Zahanati kijijini hapo.